Biblia Habari Njema

2 Wafalme 25:18-26 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Kisha Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme alimchukua mateka Seraya kuhani mkuu, Sefania kuhani wa pili pamoja na maofisa walinda milango watatu;

19. alimchukua towashi mmoja huko mjini ambaye alikuwa akiwaongoza askari vitani, pamoja na watu watano mashuhuri wa mfalme ambao aliwakuta huko. Vilevile, alimchukua katibu wa kamanda mkuu wa jeshi ambaye alitunza kumbukumbu za jeshi pamoja na watu sitini mashuhuri ambao aliwakuta mjini Yerusalemu.

20. Nebuzaradani kapteni wa walinzi aliwachukua watu hao, akawapeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla.

21. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwapiga na kuwaua watu hao huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Hivyo watu wa Yuda walichukuliwa mateka nje ya nchi yao.

22. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni alimteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, kuwa mtawala wa watu wote wa Yuda ambao hawakupelekwa Babuloni.

23. Kisha makapteni wote wa majeshi pamoja na watu wao waliposikia kuwa mfalme wa Babuloni alimteua Gedalia kuwa mtawala, walimwendea Gedalia huko Mizpa. Watu hao walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka.

24. Naye Gedalia aliapa mbele yao na watu wao, akasema, “Msiogope kwa sababu ya maofisa wa Wakaldayo. Kaeni nchini mumtumikie mfalme wa Babuloni na mambo yote yatawaendea vema.”

25. Mnamo mwezi wa saba, Ishmaeli mwana wa Nethania, mjukuu wa Elishama aliyekuwa wa ukoo wa kifalme, alifika kwa Gedalia akiandamana na watu kumi, akamshambulia Gedalia, akamuua. Vilevile, aliwaua Wayahudi na Wakaldayo waliokuwa naye.

26. Halafu, Waisraeli wote, wadogo kwa wakubwa pamoja na maofisa wa majeshi, waliondoka, wakaenda Misri, kwa sababu waliwaogopa Wakaldayo.