Biblia Habari Njema

2 Wafalme 16:6-17 Biblia Habari Njema (BHN)

6. (Wakati huo, mfalme wa Edomu aliuteka akawarudishia Waedomu mji wa Elathi na kuwafukuza watu wa Yuda waliokaa humo. Nao Waedomu wakaingia Elathi na kufanya makao yao huko mpaka sasa.)

7. Basi Ahazi akatuma watu kwa mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru wakiwa na ujumbe huu: “Mimi ni mtumishi wako mwaminifu. Njoo uniokoe kutoka kwa wafalme wa Aramu na Israeli ambao wananishambulia.”

8. Ahazi akachukua fedha na dhahabu iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na hazina iliyokuwa katika nyumba ya mfalme na kumpelekea kama zawadi mfalme wa Ashuru.

9. Tiglath-pileseri, akiitikia ombi la Ahazi, aliushambulia mji wa Damasko na kuuteka. Akamuua mfalme Resini na kuwapeleka mateka Kiri.

10. Mfalme Ahazi alipokwenda Damasko kukutana na mfalme Tiglath-pileseri, aliona madhabahu huko. Basi, akamtumia kuhani Uria mfano kamili na mchoro wa madhabahu hiyo.

11. Uria akajenga madhabahu hiyo kulingana na mfano huo na kuimaliza kabla ya Ahazi kurejea nyumbani.

12. Ahazi aliporejea kutoka Damasko, aliiona hiyo madhabahu; basi akaikaribia madhabahu na kutoa sadaka juu yake.

13. Alitoa sadaka yake ya kuteketezwa, ya nafaka, na ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka ya amani.

14. Madhabahu ya shaba ambayo iliwekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, aliiondoa mbele ya nyumba kutoka nafasi yake katikati ya madhabahu yake na nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka kwenye nafasi iliyokuwa upande wa kaskazini wa madhabahu yake.

15. Kisha alimwamuru Uria, “Tumia hii madhabahu yangu kubwa kwa kuteketeza sadaka za asubuhi na sadaka za nafaka za jioni, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka za mfalme na za watu wote na pia sadaka za divai za watu. Irashie damu ya wanyama wote wa kuteketezwa ambao wametolewa sadaka. Lakini ile madhabahu ya shaba nitaitumia mimi kwa kuuliza kauli ya Mungu.”

16. Naye Uria akafuata maagizo ya mfalme.

17. Mfalme Ahazi aliziondoa papi zilizokuwa zimesimamishwa huko, akaondoa birika lililoitwa bahari ambalo lilikuwa juu ya wale fahali kumi na wawili wa shaba na kuliweka juu ya msingi wa mawe.