Biblia Habari Njema

Yohane 7:36-46 Biblia Habari Njema (BHN)

36. Ana maana gani anaposema: ‘Mtanitafuta lakini hamtanipata, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika?’”

37. Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalumu. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, “Aliye na kiu na aje kwangu anywe.

38. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’”

39. (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado).

40. Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, “Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!”

41. Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine walisema, “Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya?

42. Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: ‘Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!’”

43. Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu.

44. Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.

45. Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, “Kwa nini hamkumleta?”

46. Walinzi wakawajibu, “Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!”