Biblia Habari Njema

Yohane 12:26-35 Biblia Habari Njema (BHN)

26. Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.

27. “Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: ‘Baba, usiruhusu saa hii inifikie?’ Lakini ndiyo maana nimekuja – ili nipite katika saa hii.

28. Baba, ulitukuze jina lako.” Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, na nitalitukuza tena.”

29. Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, “Ni ngurumo.” Lakini wengine wakasema, “Malaika ameongea naye!”

30. Lakini Yesu akawaambia, “Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu.

31. Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa.

32. Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu.”

33. (Kwa kusema hivyo alionesha atakufa kifo gani).

34. Basi, umati huo ukamjibu, “Sisi tunaambiwa na sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?”

35. Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako.