Biblia Habari Njema

Yohane 12:15-31 Biblia Habari Njema (BHN)

15. “Usiogope mji wa Siyoni!Tazama, Mfalme wako anakuja,amepanda mwanapunda!”

16. Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.

17. Kundi la watu wale waliokuwa pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka kwa wafu, walimshuhudia.

18. Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo.

19. Basi, Mafarisayo wakaambiana, “Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata.”

20. Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo.

21. Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, “Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu.”

22. Filipo akaenda, akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu.

23. Yesu akawaambia, “Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika!

24. Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi.

25. Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uhai wa milele.

26. Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.

27. “Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: ‘Baba, usiruhusu saa hii inifikie?’ Lakini ndiyo maana nimekuja – ili nipite katika saa hii.

28. Baba, ulitukuze jina lako.” Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, na nitalitukuza tena.”

29. Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, “Ni ngurumo.” Lakini wengine wakasema, “Malaika ameongea naye!”

30. Lakini Yesu akawaambia, “Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu.

31. Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa.