Biblia Habari Njema

Mhubiri 2:16-23 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Maana hakuna amkumbukaye mwenye hekima, wala amkumbukaye mpumbavu, kwani siku zijazo wote watasahaulika. Jinsi mwenye hekima afavyo ndivyo afavyo mpumbavu!

17. Kwa hiyo, nikayachukia maisha, maana yote yatendekayo duniani yalinisikitisha. Yote yalikuwa bure kabisa; nilikuwa nikifukuza upepo.

18. Nilichukia kazi yangu yote niliyokuwa nimefanya hapa duniani, kuona kwamba ilinipasa nimwachie mtu ambaye atatawala baada yangu.

19. Tena, ni nani ajuaye kwamba atakuwa mwenye hekima au atakuwa mpumbavu? Hata hivyo, yeye atamiliki yote niliyofanya kwa kutumia hekima yangu hapa duniani. Pia hayo yote ni bure kabisa.

20. Basi, nilipofikiria tena juu ya yote niliyofanya duniani, nilikata tamaa.

21. Maana, wakati mwingine mtu ambaye amefanya kazi kwa kutumia hekima, akili na maarifa yake, humwachia mtu mwingine afurahie matunda ya kazi ambayo hakuitolea jasho. Pia hilo nalo ni bure kabisa; ni jambo baya sana.

22. Mtu anafaidi nini kutokana na kazi zake zote, na juhudi anazohangaika nazo duniani?

23. Kwa sababu maisha yake yote yamejaa taabu, na kazi yake ni mahangaiko matupu; hata usiku akili yake haipumziki! Hayo nayo ni bure kabisa.