Biblia Habari Njema

Matendo 21:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa wanaongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.

5. Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali.

6. Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli, nao wakarudi makwao.

7. Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja.

8. Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu.

9. Alikuwa na binti wanne ambao walikuwa na kipaji cha unabii.

10. Baada ya kukaa huko siku kadhaa, nabii mmoja aitwaye Agabo alifika kutoka Yudea.

11. Alitujia, akachukua mkanda wa Paulo, akajifunga mikono na miguu, akasema, “Roho Mtakatifu asema hivi: ‘Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga namna hii mtu mwenye mkanda huu na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa.’”