Biblia Habari Njema

Luka 8:9-20 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Wanafunzi wake Yesu wakamwuliza maana ya mfano huo.

10. Naye akajibu, “Nyinyi mmejaliwa kujua siri za ufalme wa Mungu, lakini hao wengine sivyo; ila hao huambiwa kwa mifano, ili wakitazama wasiweze kuona, na wakisikia wasifahamu.

11. “Basi, maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu.

12. Zile zilizoanguka njiani zinaonesha watu wale wanaosikia lile neno, halafu Ibilisi akaja na kuliondoa mioyoni mwao wasije wakaamini wakaokoka.

13. Zile zilizoanguka penye mawe zinaonesha watu wale ambao wanaposikia juu ya lile neno hulipokea kwa furaha. Lakini kama zile mbegu, watu hao hawana mizizi maana husadiki kwa kitambo tu, na wanapojaribiwa hukata tamaa.

14. Zile zilizoanguka kwenye miti ya miiba ni watu wale wanaosikia lile neno, lakini muda si muda, wanapokwenda zao, husongwa na wasiwasi, mali na anasa za maisha, nao hawazai matunda yakakomaa.

15. Na zile zilizoanguka kwenye udongo mzuri ndio watu wale wanaolisikia lile neno, wakalizingatia kwa moyo mwema na wa utii. Hao huvumilia mpaka wakazaa matunda.

16. “Watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni. Lakini huiweka juu ya kinara ili watu wanapoingia ndani wapate kuona mwanga.

17. “Chochote kilichofichwa kitafichuliwa, na siri yoyote itagunduliwa na kujulikana hadharani.

18. “Kwa hiyo, jihadharini jinsi mnavyosikia; maana aliye na kitu ataongezewa, lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho, kitachukuliwa.”

19. Hapo mama na ndugu zake Yesu wakamjia, lakini hawakuweza kumkaribia kwa sababu ya umati wa watu.

20. Yesu akapewa habari kwamba mama na ndugu zake walikuwa nje, wanataka kumwona.