Biblia Habari Njema

Luka 8:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Na zile zilizoanguka kwenye udongo mzuri ndio watu wale wanaolisikia lile neno, wakalizingatia kwa moyo mwema na wa utii. Hao huvumilia mpaka wakazaa matunda.

16. “Watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni. Lakini huiweka juu ya kinara ili watu wanapoingia ndani wapate kuona mwanga.

17. “Chochote kilichofichwa kitafichuliwa, na siri yoyote itagunduliwa na kujulikana hadharani.

18. “Kwa hiyo, jihadharini jinsi mnavyosikia; maana aliye na kitu ataongezewa, lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho, kitachukuliwa.”

19. Hapo mama na ndugu zake Yesu wakamjia, lakini hawakuweza kumkaribia kwa sababu ya umati wa watu.

20. Yesu akapewa habari kwamba mama na ndugu zake walikuwa nje, wanataka kumwona.

21. Lakini Yesu akawaambia watu wote, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”

22. Siku moja, Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvuke ziwa twende mpaka ngambo.” Basi, wakaanza safari.

23. Walipokuwa wanasafiri kwa mashua, Yesu alishikwa na usingizi, akalala. Dhoruba kali ikaanza kuvuma, maji yakaanza kuingia ndani ya mashua, wakawa katika hatari.

24. Wale wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwamsha wakisema, “Bwana, Bwana! Tunaangamia!” Yesu akaamka, akaukemea upepo na mawimbi ya maji, navyo vikatulia, kukawa shwari.

25. Kisha akawaambia, “Iko wapi imani yenu?” Lakini wao walishangaa na kuogopa huku wakiambiana, “Huyu ni nani basi, hata anaamuru dhoruba na mawimbi, navyo vinamtii?”

26. Wakaendelea na safari, wakafika pwani ya nchi ya Wagerase inayokabiliana na Galilaya, ngambo ya ziwa.

27. Alipokuwa anashuka pwani, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo alimjia kutoka mjini. Kwa muda mrefu mtu huyo hakuwa anavaa nguo, wala hakuwa anaishi nyumbani bali makaburini.