Biblia Habari Njema

2 Wafalme 23:32-37 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Yehoahazi alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama babu zake walivyofanya.

33. Ili asiendelee kutawala huko Yerusalemu, Farao Neko alimtia nguvuni huko Ribla katika nchi ya Hamathi, akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za madini ya fedha na kilo 34 za dhahabu.

34. Farao Neko akamtawaza Eliakimu mwana wa mfalme Yosia mahali pa baba yake Yosia, akabadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Lakini alimchukua Yehoahazi mbali mpaka Misri na kufia huko.

35. Mfalme Yehoyakimu alimpa Farao fedha na dhahabu, lakini aliitoza nchi kodi ili aweze kutekeleza matakwa ya Farao ya kupewa fedha. Aliwatoza wananchi fedha na dhahabu. Kila mmoja alitoa kiasi alichokadiria mfalme, naye akampa Farao Neko.

36. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, na alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake lilikuwa Zebida binti Pedaya wa Ruma.

37. Yehoyakimu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama waliyoyafanya babu zake wote.