Biblia Habari Njema

2 Wafalme 16:5-12 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walitokea ili kupigana vita dhidi ya Yerusalemu, nao walimzingira Ahazi, lakini hawakuweza kumshinda.

6. (Wakati huo, mfalme wa Edomu aliuteka akawarudishia Waedomu mji wa Elathi na kuwafukuza watu wa Yuda waliokaa humo. Nao Waedomu wakaingia Elathi na kufanya makao yao huko mpaka sasa.)

7. Basi Ahazi akatuma watu kwa mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru wakiwa na ujumbe huu: “Mimi ni mtumishi wako mwaminifu. Njoo uniokoe kutoka kwa wafalme wa Aramu na Israeli ambao wananishambulia.”

8. Ahazi akachukua fedha na dhahabu iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na hazina iliyokuwa katika nyumba ya mfalme na kumpelekea kama zawadi mfalme wa Ashuru.

9. Tiglath-pileseri, akiitikia ombi la Ahazi, aliushambulia mji wa Damasko na kuuteka. Akamuua mfalme Resini na kuwapeleka mateka Kiri.

10. Mfalme Ahazi alipokwenda Damasko kukutana na mfalme Tiglath-pileseri, aliona madhabahu huko. Basi, akamtumia kuhani Uria mfano kamili na mchoro wa madhabahu hiyo.

11. Uria akajenga madhabahu hiyo kulingana na mfano huo na kuimaliza kabla ya Ahazi kurejea nyumbani.

12. Ahazi aliporejea kutoka Damasko, aliiona hiyo madhabahu; basi akaikaribia madhabahu na kutoa sadaka juu yake.