Biblia Habari Njema

2 Wafalme 15:21-29 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Matendo mengine yote ya Menahemu yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

22. Menahemu alifariki, naye mwanawe Pekahia alitawala mahali pake.

23. Katika mwaka wa hamsini wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka miwili.

24. Alimwasi Mwenyezi-Mungu na kufuata mfano mbaya wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

25. Peka mwana wa Remalia, ambaye alikuwa ofisa wa jeshi la Pekahia, alishirikiana na watu wengine hamsini kutoka Gileadi, akamuua Pekahia katika ngome ya ndani ya nyumba ya mfalme huko Samaria, na kuwa mfalme mahali pake.

26. Matendo mengine ya Pekahia na yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

27. Katika mwaka wa hamsini na mbili wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Peka mwana wa Remalia alianza kutawala huko Samaria, akatawala kwa muda wa miaka ishirini.

28. Alimwasi Mwenyezi-Mungu kwa kufuata mfano mbaya wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewafanya watu wa Israeli watende dhambi.

29. Wakati wa enzi ya Peka mfalme wa Israeli, Tiglath-pileseri, mfalme wa Ashuru, aliteka miji ya Iyoni, Abel-beth-maaka, Yanoa, Kadeshi na Hazori, pamoja na nchi za Gileadi, Galilaya na Naftali na kuwachukua mateka wakazi wao.