Biblia Habari Njema

2 Wafalme 10:15-23 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Yehu akatoka tena na alipofika njiani akakutana na Yehonadabu mwana wa Rekabu; Yehu akamsalimu, kisha akamwambia “Wewe una mawazo sawa na yangu? Je, utajiunga nami na kunisaidia?” Yehonadabu akamjibu, “Naam, nitajiunga nawe:”Yehu akasema, “Basi, nipe mkono wako.” Wakashikana mikono na Yehu akampandisha garini mwake.

16. Akamwambia, “Fuatana nami ili ujionee jinsi nilivyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu.” Basi, wakasafiri pamoja garini mwake.

17. Walipofika Samaria, Yehu aliua jamaa yote ya Ahabu bila kumwacha hata mmoja wao. Ikawa sawa kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Elia itakavyokuwa.

18. Yehu akawakusanya watu wa Samaria na kuwaambia, “Mfalme Ahabu alimtumikia Baali kidogo tu, lakini mimi nitamtumikia zaidi.

19. Waite manabii wote wa Baali, wafuasi wake wote na makuhani. Ni sharti kila mmoja afike, kwani nataka kumtolea Baali tambiko kubwa, na yeyote atakayekosa kufika atauawa.” Hiyo ilikuwa ni njama ya Yehu ili apate kuwaua wafuasi wa Baali.

20. Yehu akaamuru: “Alika mkutano mkubwa wa ibada ya Baali!” Tangazo likatolewa,

21. na Yehu akapeleka habari katika nchi yote ya Israeli ili wafuasi wote wa Baali wahudhurie kila mmoja. Wakaja wote na kujaa katika hekalu la Baali kutoka pembe moja mpaka nyingine.

22. Ndipo Yehu akamwagiza aliyesimamia mavazi matakatifu akisema, “Toa mavazi hayo na kuwapa watu waliohudhuria ibada.” Msimamizi akatoa mavazi hayo, akawapa.

23. Halafu Yehu akaingia katika hekalu la Baali akifuatana na Yehonadabu na kuwaambia waliokuwa hekaluni, “Hakikisheni kwamba waliomo hekaluni ni wale wamwabuduo Baali tu, na kwamba hakuna mtu yeyote anayemwabudu Mwenyezi-Mungu.