Biblia Habari Njema

1 Wafalme 13:17-30 Biblia Habari Njema (BHN)

17. maana, Mwenyezi-Mungu aliniamuru nisile chakula au kunywa maji mahali hapa, wala nisirudi kwa njia niliyoijia.”

18. Huyo mzee wa Betheli akamwambia, “Mimi pia ni nabii kama wewe, na Mwenyezi-Mungu amenena nami kwa njia ya malaika akisema, ‘Mrudishe nyumbani kwako, ale chakula na kunywa maji.’” Lakini huyo nabii mzee alikuwa anamdanganya tu.

19. Basi, mtu wa Mungu akarudi pamoja naye, akala chakula na kunywa maji kwa huyo mzee.

20. Walipokuwa mezani, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia huyo nabii mzee,

21. naye akamwambia kwa sauti huyo mtu wa Mungu kutoka Yuda: “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Wewe umeacha kutii ujumbe wa Mwenyezi-Mungu; wewe hukufuata amri aliyokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.

22. Badala yake, umerudi hapa, ukala chakula na kunywa maji mahali hapa ambapo uliambiwa usile chakula wala kunywa maji. Basi, mwili wako hautazikwa kwenye kaburi la babu zako.’”

23. Walipomaliza kula, huyo nabii mzee akamtandikia punda huyo mtu wa Mungu, naye akaondoka.

24. Alipokuwa anakwenda zake, simba akakutana naye njiani, akamuua; mwili wake ukawa umetupwa hapo barabarani; punda wake na huyo simba wakawa wamesimama kando yake.

25. Watu waliopitia hapo na kuiona maiti barabarani, na simba amesimama karibu nayo, wakaenda mpaka mjini alimokuwa anakaa yule nabii, wakawaambia watu.

26. Nabii yule ambaye alikuwa amemkaribisha nyumbani kwake aliposikia habari hiyo, akasema, “Huyo ni yuleyule mtu wa Mungu aliyekataa kutii neno la Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu amemtuma simba, akamshambulia na kumwua kama alivyokuwa amemwambia.”

27. Hapo akawaambia wanawe “Nitandikie punda.” Nao wakamtandikia.

28. Mzee akaenda, akaikuta maiti ya mtu wa Mungu barabarani, simba na punda wake kando yake; huyo simba hakuila maiti wala hakumshambulia punda.

29. Basi, huyo nabii mzee akaitwaa maiti ya mtu wa Mungu, akaiweka juu ya punda wake, akairudisha mjini Betheli, kuomboleza kifo chake na kumzika.

30. Basi, akamzika katika kaburi lake, naye pamoja na wanawe wakaomboleza kifo chake wakisema, “Aa! Ndugu yangu!”