Biblia Habari Njema

Yohane 9:12-31 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Wakamwuliza, “Yeye yuko wapi?” Naye akawajibu, “Mimi sijui!”

13. Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo.

14. Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato.

15. Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, “Umepataje kuona?” Naye akawaambia, “Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona.”

16. Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato.” Lakini wengine wakasema, “Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?” Kukawa na mafarakano kati yao.

17. Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, “Maadamu yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?” Naye akawaambia, “Yeye ni nabii!”

18. Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona, mpaka walipowaita wazazi wake.

19. Basi, wakawauliza hao wazazi, “Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye nyinyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?”

20. Wazazi wake wakajibu, “Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu.

21. Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe.”

22. Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi.

23. Ndiyo maana wazazi wake walisema: “Yeye ni mtu mzima, mwulizeni.”

24. Basi, wakamwita tena huyo aliyekuwa kipofu, wakamwambia, “Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi.”

25. Yeye akajibu, “Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona.”

26. Basi, wakamwuliza, “Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?”

27. Huyo mtu akawajibu, “Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, nyinyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?”

28. Lakini wao wakamtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose.

29. Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!”

30. Naye akawajibu, “Hili ni jambo la kushangaza! Nyinyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu!

31. Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake.