Biblia Habari Njema

Yohane 9:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa.

2. Basi, wanafunzi wakamwuliza, “Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: Mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?”

3. Yesu akajibu, “Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake.

4. Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi.

5. Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu.”

6. Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni,

7. akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Maana ya jina hili ni “aliyetumwa”). Hapo, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona.

8. Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, “Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?”

9. Baadhi yao wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “La! Ila anafanana naye.” Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, “Ni mimi!”