Biblia Habari Njema

Yohane 8:49-59 Biblia Habari Njema (BHN)

49. Yesu akajibu, “Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini nyinyi hamniheshimu.

50. Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu.

51. Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele.”

52. Basi, Wayahudi wakasema, “Sasa tunajua kweli kwamba wewe una pepo! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, ‘Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele!’

53. Je, unajifanya mkuu kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?”

54. Yesu akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye nyinyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza.

55. Nyinyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama nyinyi. Mimi namjua na ninashika neno lake.

56. Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi.”

57. Basi, Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?”

58. Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko.”

59. Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.