Biblia Habari Njema

Yohane 8:24-36 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, mtakufa katika dhambi zenu.”

25. Nao wakamwuliza, “Wewe ni nani?” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni tangu mwanzo!

26. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake.”

27. Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.

28. Basi, Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu, hapo ndipo mtakapojua kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha.

29. Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza.”

30. Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini.

31. Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.

32. Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru.”

33. Nao wakamjibu, “Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: ‘Mtakuwa huru?’”

34. Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.

35. Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu.

36. Mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli.