Biblia Habari Njema

Yohane 8:21-29 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Yesu akawaambia tena, “Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, nyinyi hamwezi kufika.”

22. Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Mbona anasema: ‘Niendako nyinyi hamwezi kufika?’”

23. Yesu akawaambia, “Nyinyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; nyinyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.

24. Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, mtakufa katika dhambi zenu.”

25. Nao wakamwuliza, “Wewe ni nani?” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni tangu mwanzo!

26. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake.”

27. Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.

28. Basi, Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu, hapo ndipo mtakapojua kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha.

29. Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza.”