Biblia Habari Njema

Yohane 8:15-25 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Nyinyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.

16. Hata nikihukumu, hukumu yangu ni halali kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.

17. Imeandikwa katika sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.

18. Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia.”

19. Hapo wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu, “Nyinyi hamnijui mimi wala hammjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia.”

20. Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.

21. Yesu akawaambia tena, “Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, nyinyi hamwezi kufika.”

22. Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Mbona anasema: ‘Niendako nyinyi hamwezi kufika?’”

23. Yesu akawaambia, “Nyinyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; nyinyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.

24. Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, mtakufa katika dhambi zenu.”

25. Nao wakamwuliza, “Wewe ni nani?” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni tangu mwanzo!