Biblia Habari Njema

Yohane 8:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, “Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?”

11. Huyo mwanamke akamjibu, “Bwana, hakuna hata mmoja!” Naye Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena.”]

12. Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uhai.”

13. Basi, Mafarisayo wakamwambia, “Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali.”

14. Yesu akawajibu, “Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini nyinyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.

15. Nyinyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.

16. Hata nikihukumu, hukumu yangu ni halali kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.

17. Imeandikwa katika sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.

18. Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia.”

19. Hapo wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu, “Nyinyi hamnijui mimi wala hammjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia.”

20. Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.