Biblia Habari Njema

Yohane 8:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni.

2. Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha.

3. Basi, waalimu wa sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao.

4. Kisha wakamwuliza Yesu, “Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi.

5. Katika sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?”

6. Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole.

7. Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, “Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe.”

8. Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini.

9. Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitangulia wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale.

10. Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, “Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?”

11. Huyo mwanamke akamjibu, “Bwana, hakuna hata mmoja!” Naye Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena.”]