Biblia Habari Njema

Yohane 7:2-17 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Sikukuu ya Wayahudi ya vibanda ilikuwa imekaribia.

3. Basi, ndugu zake wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya.

4. Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadamu unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu.”

5. (Hata ndugu zake hawakumwamini).

6. Basi, Yesu akawaambia, “Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu nyinyi kila wakati unafaa.

7. Ulimwengu hauwezi kuwachukia nyinyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nashuhudia juu yake kwamba matendo yake ni maovu.

8. Nyinyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika.”

9. Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya.

10. Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri.

11. Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; wakauliza, “Yuko wapi?”

12. Kulikuwa na minongono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.”

13. Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.

14. Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda hekaluni, akaanza kufundisha.

15. Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?”

16. Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.

17. Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.