Biblia Habari Njema

Yohane 6:43-59 Biblia Habari Njema (BHN)

43. Yesu akawaambia, “Acheni kunungunika nyinyi kwa nyinyi.

44. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo siku ya mwisho.

45. Manabii wameandika: ‘Watu wote watafundishwa na Mungu.’ Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu.

46. Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.

47. Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uhai wa milele.

48. Mimi ni mkate wa uhai.

49. Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa.

50. Lakini huu ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni ili yeyote atakayeula asife.

51. Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.”

52. Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?”

53. Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu.

54. Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uhai wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho.

55. Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.

56. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake.

57. Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu.

58. Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zenu, wakafa. Aulaye mkate huu atakuwa hai milele.”

59. Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu.