Biblia Habari Njema

Yohane 6:32-40 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye nyinyi mkate wa kweli kutoka mbinguni.

33. Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uhai.”

34. Basi, wakamwambia, “Bwana, tupe daima mkate huo.”

35. Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.

36. Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini.

37. Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu,

38. kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.

39. Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: Nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote siku ya mwisho.

40. Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: Kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uhai wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”