Biblia Habari Njema

Yohane 6:23-40 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu.

24. Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta.

25. Wale watu walipomkuta Yesu ngambo ya pili wa ziwa walimwuliza, “Mwalimu, ulifika lini hapa?”

26. Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.

27. Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishughulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uhai wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho.”

28. Wao wakamwuliza, “Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?”

29. Yesu akawajibu, “Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu mwifanye: Kumwamini yule aliyemtuma.”

30. Hapo wakamwambia, “Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani?

31. Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: ‘Aliwalisha mkate kutoka mbinguni.’”

32. Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye nyinyi mkate wa kweli kutoka mbinguni.

33. Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uhai.”

34. Basi, wakamwambia, “Bwana, tupe daima mkate huo.”

35. Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.

36. Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini.

37. Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu,

38. kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.

39. Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: Nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote siku ya mwisho.

40. Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: Kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uhai wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”