Biblia Habari Njema

Yohane 6:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Yesu akasema, “Waketisheni watu.” Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume 5,000.

11. Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka.

12. Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee.”

13. Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili.

14. Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, “Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni.”

15. Yesu akajua kwamba watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake.

16. Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani,

17. wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado.

18. Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.

19. Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana.

20. Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope!”