Biblia Habari Njema

Yohane 5:21-40 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uhai, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uhai wale anaopenda.

22. Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana,

23. ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.

24. “Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uhai wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifoni na kuingia katika uhai.

25. Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi.

26. Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai.

27. Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu.

28. Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake,

29. nao watafufuka: Wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa.

30. “Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi ninahukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.

31. Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli.

32. Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli.

33. Nyinyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli.

34. Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa.

35. Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo.

36. Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma.

37. Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Nyinyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake,

38. na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma.

39. Nyinyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uhai wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia!

40. Hata hivyo, nyinyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uhai.