Biblia Habari Njema

Yohane 5:18-30 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumuua Yesu; si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.

19. Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile.

20. Baba ampenda Mwana, na humwonesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu.

21. Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uhai, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uhai wale anaopenda.

22. Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana,

23. ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.

24. “Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uhai wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifoni na kuingia katika uhai.

25. Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi.

26. Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai.

27. Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu.

28. Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake,

29. nao watafufuka: Wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa.

30. “Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi ninahukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.