Biblia Habari Njema

Yohane 5:15-23 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya.

16. Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu.

17. Basi, Yesu akawaambia, “Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi.”

18. Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumuua Yesu; si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.

19. Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile.

20. Baba ampenda Mwana, na humwonesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu.

21. Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uhai, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uhai wale anaopenda.

22. Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana,

23. ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.