Biblia Habari Njema

Yohane 5:11-18 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Lakini yeye akawaambia, “Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: ‘Chukua mkeka wako, utembee.’”

12. Nao wakamwuliza, “Huyo mtu aliyekuambia: ‘Chukua mkeka wako, utembee,’ ni nani?”

13. Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu.

14. Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa hekaluni, akamwambia, “Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi.”

15. Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya.

16. Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu.

17. Basi, Yesu akawaambia, “Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi.”

18. Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumuua Yesu; si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.