Biblia Habari Njema

Yohane 5:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu.

2. Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao.

3. Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: Vipofu, viwete na waliopooza. [Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe,

4. maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.]

5. Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane.

6. Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo na kujua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, “Je, wataka kupona?”

7. Naye akajibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia.”

8. Yesu akamwambia, “Inuka, chukua mkeka wako utembee.”

9. Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.

10. Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako.”

11. Lakini yeye akawaambia, “Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: ‘Chukua mkeka wako, utembee.’”

12. Nao wakamwuliza, “Huyo mtu aliyekuambia: ‘Chukua mkeka wako, utembee,’ ni nani?”

13. Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu.

14. Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa hekaluni, akamwambia, “Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi.”

15. Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya.