Biblia Habari Njema

Yohane 4:3-11 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya;

4. na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria.

5. Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu.

6. Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.

7. Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, “Nipatie maji ninywe.”

8. (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)

9. Lakini huyo mwanamke akamwambia, “Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?” (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu).

10. Yesu akamjibu, “Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekuambia: ‘Nipatie maji ninywe,’ ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yenye uhai.”

11. Huyo mama akasema, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yenye uhai?