Biblia Habari Njema

Yohane 4:24-35 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Mungu ni roho, na watu wanaomwabudu lazima wamwabudu kwa Roho na ukweli.”

25. Huyo mama akamwambia, “Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu.”

26. Yesu akamwambia, “Mimi ninayeongea nawe, ndiye.”

27. Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: “Unataka nini?” au, “Kwa nini unaongea na mwanamke?”

28. Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,

29. “Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?”

30. Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.

31. Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, kula chakula.”

32. Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua nyinyi.”

33. Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?”

34. Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.

35. Nyinyi mwasema: ‘Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!’ Lakini mimi nawaambieni, angalieni mkaone jinsi mashamba yalivyo tayari kuvunwa.