Biblia Habari Njema

Yohane 4:16-29 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Yesu akamwambia, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.”

17. Huyo mwanamke akamwambia, “Mimi sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli, kwamba huna mume.

18. Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli.”

19. Huyo Mwanamke akamwambia, “Bwana, naona ya kuwa wewe u nabii.

20. Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini nyinyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudia Mungu ni kule Yerusalemu.”

21. Yesu akamwambia, “Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu.

22. Nyinyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi.

23. Lakini wakati waja, tena umekwisha wasili, ambapo wenye kuabudu wa kweli watamwabudu Baba katika roho na ukweli. Maana Baba anawataka watu wanaomwabudu namna hiyo.

24. Mungu ni roho, na watu wanaomwabudu lazima wamwabudu kwa Roho na ukweli.”

25. Huyo mama akamwambia, “Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu.”

26. Yesu akamwambia, “Mimi ninayeongea nawe, ndiye.”

27. Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: “Unataka nini?” au, “Kwa nini unaongea na mwanamke?”

28. Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,

29. “Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?”