Biblia Habari Njema

Yohane 3:26-36 Biblia Habari Njema (BHN)

26. Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, “Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ngambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea.”

27. Yohane akawaambia, “Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu.

28. Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: ‘Mimi siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!’

29. Bibi arusi ni wake bwana arusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa.

30. Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue.”

31. Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wote.

32. Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali ujumbe wake.

33. Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu ni kweli.

34. Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia mtu huyo Roho wake bila kipimo.

35. Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote.

36. Anayemwamini Mwana anao uhai wa milele; asiyemwamini Mwana hatakuwa na uhai wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake.