Biblia Habari Njema

Yohane 3:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

15. ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele.

16. Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele.

17. Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe.

18. “Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa, kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu.

19. Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu.

20. Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe.

21. Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu.”

22. Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake. Alikaa huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu.

23. Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza.

24. (Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.)

25. Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja kuhusu desturi za kutawadha.

26. Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, “Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ngambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea.”

27. Yohane akawaambia, “Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu.