Biblia Habari Njema

Yohane 21:15-20 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, “Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi kuliko hawa?” Naye akajibu, “Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda.” Yesu akamwambia, “Tunza wanakondoo wangu.”

16. Kisha akamwambia mara ya pili, “Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?” Petro akamjibu, “Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda.” Yesu akamwambia, “Tunza kondoo wangu.”

17. Akamwuliza mara ya tatu, “Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?” Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: “Wanipenda?” Akamwambia, “Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda.” Yesu akamwambia, “Tunza kondoo wangu!

18. Kweli nakuambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda.”

19. (Kwa kusema hivyo, alionesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu). Kisha akamwambia, “Nifuate.”

20. Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata (Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: “Bwana ni nani atakayekusaliti?”)