Biblia Habari Njema

Yohane 2:17-25 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: “Upendo wangu kwa nyumba yako waniua.”

18. Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, “Utafanya mwujiza gani kuonesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?”

19. Yesu akawaambia, “Vunjeni hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu.”

20. Hapo Wayahudi wakasema, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arubaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?”

21. Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya hekalu ambalo ni mwili wake.

22. Basi, alipofufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakayaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno ambayo Yesu alikuwa amesema.

23. Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizofanya.

24. Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote.

25. Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.