Biblia Habari Njema

Yohane 2:11-24 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.

12. Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache.

13. Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda juu Yerusalemu.

14. Basi, akawakuta mle hekaluni watu wakiuza ng'ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.

15. Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya hekalu pamoja na kondoo na ng'ombe wao, akazitawanya sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao.

16. Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, “Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!”

17. Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: “Upendo wangu kwa nyumba yako waniua.”

18. Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, “Utafanya mwujiza gani kuonesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?”

19. Yesu akawaambia, “Vunjeni hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu.”

20. Hapo Wayahudi wakasema, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arubaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?”

21. Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya hekalu ambalo ni mwili wake.

22. Basi, alipofufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakayaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno ambayo Yesu alikuwa amesema.

23. Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizofanya.

24. Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote.