Biblia Habari Njema

Yohane 18:8-17 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Yesu akawaambia, “Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye. Basi, kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” (

9. Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: “Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.”)

10. Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la kulia mtumishi wa kuhani mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko.

11. Basi, Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako alani. Je, nisinywe kikombe cha mateso alichonipa Baba?”

12. Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga

13. na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo.

14. Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.

15. Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa kuhani mkuu.

16. Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa kuhani mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, mngojamlango, akamwingiza Petro ndani.

17. Huyo mjakazi mngojamlango akamwuliza Petro, “Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akamwambia, “Si mimi!”