Biblia Habari Njema

Yohane 18:31-40 Biblia Habari Njema (BHN)

31. Pilato akawaambia, “Haya, mchukueni nyinyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na sheria yenu.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu yeyote.” (

32. Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonesha atakufa kifo gani.)

33. Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: “Ati wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?”

34. Yesu akamjibu, “Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekuambia habari zangu?”

35. Pilato akamjibu, “Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako na makuhani wamekuleta kwangu. Umefanya nini?”

36. Yesu akamjibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini sasa ufalme wangu si wa hapa.”

37. Hapo Pilato akamwambia, “Basi, wewe ni Mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe umesema kwamba mimi ni Mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili hiyo; na kwa ajili hiyo nimekuja ulimwenguni kuwaambia watu juu ya ukweli. Kila mtu wa ukweli hunisikiliza.”

38. Pilato akamwambia, “Ukweli ni kitu gani?”Pilato alipokwisha sema hayo, aliwaendea tena Wayahudi nje, akawaambia, “Mimi sioni hatia yoyote kwake.

39. Lakini, mnayo desturi kwamba mimi niwafungulie mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Basi, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?”

40. Hapo wakapiga kelele: “La! Si huyu ila Baraba!” Naye Baraba alikuwa mnyanganyi.