Biblia Habari Njema

Yohane 18:24-35 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa kuhani mkuu Kayafa.

25. Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, “Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?” Yeye akakana na kusema, “Si mimi!”

26. Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, “Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?”

27. Petro akakana tena; mara jogoo akawika.

28. Basi, walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu. Ilikuwa alfajiri, nao ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije wakatiwa unajisi.

29. Kwa hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, “Mna mashtaka gani juu ya mtu huyu?”

30. Wakamjibu, “Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako.”

31. Pilato akawaambia, “Haya, mchukueni nyinyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na sheria yenu.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu yeyote.” (

32. Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonesha atakufa kifo gani.)

33. Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: “Ati wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?”

34. Yesu akamjibu, “Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekuambia habari zangu?”

35. Pilato akamjibu, “Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako na makuhani wamekuleta kwangu. Umefanya nini?”