Biblia Habari Njema

Yohane 18:17-31 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Huyo mjakazi mngojamlango akamwuliza Petro, “Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akamwambia, “Si mimi!”

18. Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.

19. Basi, kuhani mkuu akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake.

20. Yesu akamjibu, “Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na hekaluni, mahali wanapokutana Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri.

21. Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao wanajua niliyowaambia.”

22. Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga kofi akisema, “Je, ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?”

23. Yesu akamjibu, “Kama nimesema vibaya, onesha huo ubaya; lakini ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?”

24. Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa kuhani mkuu Kayafa.

25. Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, “Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?” Yeye akakana na kusema, “Si mimi!”

26. Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, “Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?”

27. Petro akakana tena; mara jogoo akawika.

28. Basi, walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu. Ilikuwa alfajiri, nao ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije wakatiwa unajisi.

29. Kwa hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, “Mna mashtaka gani juu ya mtu huyu?”

30. Wakamjibu, “Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako.”

31. Pilato akawaambia, “Haya, mchukueni nyinyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na sheria yenu.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu yeyote.” (