Biblia Habari Njema

Yohane 18:12-21 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga

13. na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo.

14. Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.

15. Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa kuhani mkuu.

16. Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa kuhani mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, mngojamlango, akamwingiza Petro ndani.

17. Huyo mjakazi mngojamlango akamwuliza Petro, “Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akamwambia, “Si mimi!”

18. Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.

19. Basi, kuhani mkuu akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake.

20. Yesu akamjibu, “Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na hekaluni, mahali wanapokutana Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri.

21. Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao wanajua niliyowaambia.”