Biblia Habari Njema

Yohane 16:5-16 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: ‘Unakwenda wapi?’

6. Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu.

7. Lakini, nawaambieni ukweli: Afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu.

8. Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu.

9. Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini;

10. kuhusu uadilifu, kwa sababu nakwenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena;

11. kuhusu hukumu, kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.

12. “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili.

13. Lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja.

14. Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawajulisheni yale atakayopata kutoka kwangu.

15. Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho atawajulisheni yale atakayopata kutoka kwangu.

16. “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!”