Biblia Habari Njema

Yohane 16:19-33 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, “Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’

20. Nawaambieni kweli, nyinyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi; mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.

21. Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani.

22. Nyinyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu.

23. Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni.

24. Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike.

25. “Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba.

26. Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu;

27. maana yeye mwenyewe anawapenda nyinyi, kwa sababu nyinyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.

28. Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba.”

29. Basi, wanafunzi wake wakamwambia, “Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo.

30. Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu.”

31. Yesu akawajibu, “Je, mnaamini sasa?

32. Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo nyinyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami.

33. Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”