Biblia Habari Njema

Yohane 16:16-23 Biblia Habari Njema (BHN)

16. “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!”

17. Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, “Ana maana gani anapotuambia: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’ Tena anasema: ‘Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!’”

18. Basi, wakawa wanaulizana, “Ana maana gani anaposema: ‘Bado kitambo kidogo?’ Hatuelewi anasema nini.”

19. Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, “Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’

20. Nawaambieni kweli, nyinyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi; mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.

21. Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani.

22. Nyinyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu.

23. Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni.