Biblia Habari Njema

Yohane 16:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu.

2. Watu watawafukuza nyinyi katika masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua nyinyi atadhani anamhudumia Mungu.

3. Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi.

4. Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni.“Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.

5. Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: ‘Unakwenda wapi?’

6. Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu.

7. Lakini, nawaambieni ukweli: Afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu.

8. Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu.

9. Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini;

10. kuhusu uadilifu, kwa sababu nakwenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena;

11. kuhusu hukumu, kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.

12. “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili.

13. Lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja.