Biblia Habari Njema

Yohane 15:11-23 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike.

12. Hii ndiyo amri yangu: Pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda nyinyi.

13. Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.

14. Nyinyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.

15. Nyinyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita nyinyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu.

16. Nyinyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapeni chochote mnachomwomba kwa jina langu.

17. Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: Pendaneni.

18. “Kama ulimwengu ukiwachukia nyinyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla ya kuwachukia nyinyi.

19. Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda nyinyi kama watu wake. Lakini kwa vile nyinyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni.

20. Kumbukeni niliyowaambieni: Mtumishi si mkuu kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na nyinyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia.

21. Lakini hayo yote watawatendeeni nyinyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma.

22. Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi.

23. Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia.